3 Septemba 2025 - 23:36
Source: Parstoday
Makubaliano ya Iran na China; njia ya kuondokana na uchukuaji maamuzi ya upande mmoja

Katika kikao chao, Marais wa Iran na China, Masoud Pezeskian na Xi Jinping wameashiria uwezo, misingi na matakwa ya viongozi wa nchi hizo mbili ya kupanua ushirikiano, na kusisitiza maslahi na utayari wao wa kuboresha uhusiano kwa kuangalia mustakabali, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa kiwango cha juu zaidi wa makubaliano ya kimkakati ya miaka 25 kati yao.

Siku ya Jumanne, Septemba 2, Rais wa Iran alisema katika kikao chake na Rais wa China: "Tuko tayari kushirikiana ili kutekeleza vipengee vyote vya makubaliano ya kimkakati ya miaka 25 kati ya nchi hizo mbili, na tunaweza kuweka malengo kusudiwa kwenye ajenda yetu kwa kufuata taratibu zinazohitajika."

Rais Pezeshkian sambamba na kueleza kuwa, tuko tayari kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwa hali yoyote ile ili uhusiano wa Iran na China uweze kuinuliwa hadi kufikia kiwango cha juu zaidi alibainisha kwamba, "Ili kuendeleza siasa zake za upande mmoja, Marekani inajipa haki ya  kuivamia nchi mbalimbali, na sasa haina tena mipaka yoyote kuhusiana na suala hilo."

Katika kikao hicho Rais wa China pia amesisitiza kuwa, tuko tayari kuendeleza uhusiano wetu na Iran kwa kuangalia mustakabali na kuongeza kuwa: "Kuharakisha utekelezaji wa makubaliano ya awali kati ya nchi hizo mbili kunaweza kutekelezwa; China iko tayari na inapenda kupanua ushirikiano na Iran katika nyanja mbalimbali."

Xi Jinping ametaja mashambulio  (ya Marekani na Israel) dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni ukiukaji wa wazi wa kanuni na sheria za kimataifa na kusema: Kamwe nguvu si njia ya kutatua matatizo.

Rais wa China ameongeza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mshirika wetu wa kistratijia, na ni lazima tushirikiane kwa dhati ili kuimarisha Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai kwa shabaha ya kukabiliana na misimamo ya upande mmoja."

Makubaliano ya Iran na China; njia ya kuondokana na uchukuaji maamuzi ya upande mmoja

Wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai katika mkutano wao nchini China

Xi Jinping pia ameeleza kuwa, tunazingatia haki na uadilifu na tunatambua haki halali za Iran za matumizi ya nishati nyuklia kwa njia ya amani na kusema: "Katika miaka ya hivi karibuni, licha ya vikwazo vya Marekani na nchi za Magharibi, tumeandaa mazingira ya kushirikiana na kwa sasa tuko tayari kupanua uhusiano wetu katika nyanja zote, hasa katika nyanja ya usafiri.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambaye alikuwa amesafiri nchini China kwa mwaliko wa mwenzake wa China kuhudhuria Mkutano wa 25 wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na Shanghai Plus, pamoja na Gwaride la Vikosi vya Wanajeshi kuadhimisha miaka 80 ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia, ameondoka Beijing kurejea Tehran baada ya kukamilisha safari yake.

Marais wa Iran na China wamesisitiza katika kikao chao umuhimu wa ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kiusalama na pia kutekelezwa kwa mapatano ya kimkakati ya miaka 25. Utekelezaji wa makubaliano hayo kati ya Iran na China una umuhimu wa pekee kutokana na mitazamo kadhaa ya kimkakati. Makubaliano haya si hati ya ushirikiano wa muda mrefu pekee, bali yanaweza pia kutayarisha njia mpya ya maingiliano ya kimataifa ya Iran katika zama za vikwazo na mashinikizo ya Marekani na serikali za Magharibi.

China mara kadhaa imeelezea upinzani wake kwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na kuunga mkono haki halali za Iran katika uwanja wa nyuklia. Ushirikiano huu unaweza kuisaidia Iran kupata njia mbadala za kiuchumi na kidiplomasia mbele ya mashinikizo ya Magharibi.

Makubaliano ya Iran na China; njia ya kuondokana na uchukuaji maamuzi ya upande mmoja

Marais wa Iran na China

China inaichukulia Iran kama "mshirika wake wa kimkakati" na inataka kupanua uhusiano katika nyanja zote, pamoja na biashara na usalama wa kikanda. Mkataba huu unaweza kuinua uhusiano wa nchi hizo mbili hadi kuunda muungano wa kimkakati wa kudumu.

Iran na China zinashirikiana kwa karibu katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, na utekelezaji wa makubaliano haya unaweza kuimarisha nafasi ya Iran katika jumuiya hiyo. Utekelezaji wa makubaliano ya kimkakati ya miaka 25 unaweza kuisaidia Iran kufuata njia ya maendeleo endelevu, uhuru wa kiuchumi, na ushirikiano wa kimataifa kwa nguvu kubwa kupitia ushirikiano mkubwa na wa kina zaidi na nchi huru.

Mashauriano ya Rais Pezeshkian na Rais wa China yanaonyesha azma kubwa ya viongozi wa Tehran na Beijing ya kuharakisha na kupanua ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kiusalama, ambao pia utakuwa na athari kwa maendeleo ya kikanda na kimataifa.

Your Comment

You are replying to: .
captcha